Zubby apuuza kisa chake na Nnadiekwe, apanga sherehe

Zubby hajasema lolote baada ya kuonekana kwenye video akimpiga mwenzake teke iliyomsababishia maumivu makubwa.

Marion Bosire
1 Min Read
Zubby Michael

Mwigizaji wa Nollywood Zubby Michael ameonekana kupuuza kisa kati yake na mwigizaji mwenza Godwin Nnadiekwe na anaripotiwa kuendeleza mipango ya sherehe ya maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa.

Kulingana na mwanablogu Tunde Ednut, Michael atahudhuria pia sherehe ya siku ya kuzaliwa ya Macro Boss lady katika eneo la Cotonou Juni 13, 2025 ambapo pia ataandaa sherehe yake ya siku ya kuzaliwa kwa mara ya kwanza.

Zubby Michael alionekana kwenye video akimpiga teke kifuani Nnadiekwe walipokuwa wakiendelea na kazi yao ya uigizaji ya kuandaa filamu.

Nnadiekwe alitangaza kisa hicho mitandaoni akisema aliumia sana kiasi cha kuvuja damu kwa ndani na amelazwa hospitalini ambapo anagharamia matibabu yake.

Zubby Michael hajasema lolote kuhusu kisa hicho huku chama cha kitaifa cha waigizaji nchini Nigeria AGN kikiahidi kufanya uchunguzi na kuchukua hatua zinazofaa.

Mwandaaji wa filamu ambaye anajiita Stanley Ontop alisema aliwasiliana na Rais wa chama hicho cha AGN Emeka Rollas ambaye alimhakikishia kwamba sula hilo litashughulikiwa.

Ontop alisema Rollas alimwitisha nambari za simu za waigizaji husika, mwandaaji wa filamu iliyokuwa ikinakiliwa, mwelekezi wake na hospitali aliyolazwa Nnadiekwe.

Kisa hicho kimesababisha wadau kadhaa watoe wito kwa kampuni za kuandaa filamu nchini nigeria ziwekeze pakubwa katika usalama wa wahusika wanapokuwa kazini.

Share This Article