Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameelezea matumaini kwamba vita kati ya Ukraine na Urusi vilivyodumu miaka vitamalizika mwaka huu.
“Tunatumai kuwa tunaweza kumaliza vita mwaka huu kwa kuwa vimekuwa vigumu sana kwa taifa zima,” alisema Zelensky.
Zelensky aliyasema hayo katika mkutano wa kilele wa viongozi wa Ulaya, pamoja na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, ambao walikuwa Kyiv kuonyesha uungaji mkono wao kwa taifa hilo.
Hata hivyo, Rais huyo alionya kuwa Ukraine inahitaji dhamana ya usalama ili kuizuia Moscow kurejea, akipendekeza uanachama wa EU na Nato kwa nchi yake utasaidia.
Urusi imepinga mara kwa mara wazo la Ukraine kujiunga na Nato.
Hapo awali, Zelensky alisema makubaliano ya amani na Urusi yanaweza kuanza kwa ubadilishanaji kamili wa wafungwa wa vita.