Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kwamba hatua ya Urusi ya kukataa kukubali mpango wa kusitisha vita inafanya iwe vigumu kukomesha vita hivyo.
Katika ujumbe aliochapisha kwenye mtandao wa X, Zelensky alilalamika kwamba Urusi pia haitoi suluhisho lolote na haijaashiria wakati itakomesha mauaji.
Jumatatu kiongozi huyo wa Ukraine anatarajiwa kusafiri hadi Washington DC atakapokutana na Rais Donald Trump ambaye anatarajiwa kumshawishi akubali mpango wa kusitisha vita.
Trump tayari ameashiria kwamba anataka kukwepa makubaliano ya kusitisha vita nchini Ukraine na kuangazia makubaliano ya kudumu ya amani.
Baada ya kukutana na Rais wa Russia Vladimir Putin Ijumaa, Rais huyo wa Marekani alisema kwenye mtandao wa Truth Social kwamba hiyo ndiyo itakuwa njia bora ya kukomesha uhasama kati ya Russia na Ukraine kwani mipango ya kusitisha vita huwa haidumu.
Alibadili mawazo kwani awali kabla ya kukutana na Putin, Trump alikuwa amesema kwamba alichokuwa akitaka ni mpango wa haraka wa kusitisha mapigano.
Katika mawasiliano kwa njia ya simu na Trump punde baada ya mkutano wake na Putin, Zelensky alitaka maafikiano ya ukweli na ya kudumu ya amani akiongeza kwamba mapigano ni lazima yasitishwe na hivyo kukomesha mauaji.
Zelensky aliorodhesha mambo kadhaa ambayo angependa yafanyike katika maafikiano hayo kama vile kurejeshwa kwa watoto walioshikwa mateka kutoka Ukraine na hakikisho la ukweli la usalama.
Inaripotiwa kwamba Putin alimpa Trump mahitaji yake kabla ya kusitisha mapigano nchini Ukraine na yanajumuisha kutwaa maeneo ya Donbas kama Donetsk.