Mwigizaji na mwandaaji filamu wa Nigeria Yul Edochie anaripotiwa kuwa na mpenzi mwingine wakati ambapo kuna uvumi kwamba anazozana na mkewe wa pili Judy Austin.
Taarifa hizo zimetolewa na mwanablogu Ajemba Stanley Chibueze maarufu kama Stanley Ontop ambaye pia ni mwandaaji wa filamu nchini Nigeria.
Kupitia Instagram na bila kutumia majina halisi ya Yul na Judy bali majina wanayotumia kujipigia debe mitandaoni, alidai kwamba familia ya mzee Pete Edochie imejitenga na Yul.
Hatua hiyo kulingana naye imetokana na aibu ambayo anawapatia kutokana na ndoa zake.
Aliendelea kudai kwamba Yul Edochie anakaribia kumwacha Judy Austin huku akiwa na uhusiano na mwanamke mwingine ambaye hakumtaja.
Haya yanajiri miezi michache tu baada ya OnTop kuibua madai ya kuwepo shida katika ndoa ya Yul Edochie na Judy Austin, matatizo yaliyosababishwa na mmoja wa watoto wao.
Wiki chache zilizopita, sauti za wanandoa hao wakigombana zilisambaa mitandaoni na kusababisha uvumi kuhusu kuvunjika kwa ndoa yao kuaminika.
Yul alikuwa na mke wa kwanza May Edochie ambaye aliamua kukatiza uhusiano naye baada yake kutangaza Judy Austin kuwa mke wake wa pili.
May alielezea kwamba hatua yake ilichochewa na kutotaka kuwa kwenye ndoa ya wake wengi. Aliripotiwa kuanzisha taratibu za talaka mahakamani lakini bado hazijatimia na bado anatumia jina Edochie.