Mwigizaji tajika wa Nollywood nchini Nigeria Yul Edochie anadaiwa kutoroka nyumbani kwake anakoishi na mke wake wa pili Judy Austin mjini Abuja nchini Nigeria.
Haya ni kulingana na mwandaaji wa filamu Ajemba Stanley Chibueze, maarufu kama Stanley Ontop aliyechapisha habari hizo kwenye Instagram.
Alielezea kwamba Yul alitoroka nyumbani akaenda kuishi hotelini kutokana na kutoelewana kati yake na Judy Austin.
Ontop anasema Yul Edochie anamlaumu Judy kwa shida zinazokumba ndoa yao. Mwigizaji huyo anaripotiwa kumlaumu mkewe wa pili kwa kifo cha mwanawe wa kiume aliyejaliwa na mkewe wa kwanza May Yul Edochie na kuvunjika kwa ndoa hiyo yake ya kwanza.
Katika chapisho lake kwenye Instagram, Ontop alitania kwamba huenda mtu aliharibu vifaa vya ushirikina alivyotumia Judy kumnasa Yul Edochie.
Aliendelea kusema kwamba Yul na Judy ambao wanafahamika kwa kuchapisha maudhui ya pamoja mitandaoni huku wakidhihirisha wanavyopendana, hawajachapisha maudhui kama hayo kwa muda.
Stanley alifichua pia kwamba binti ya Yul na May Edochie aitwaye Danielle alimfungia babake kwenye mitandao ya kijamii na inaonekana kwamba hayuko tayari kumsamehe babake kwa kuwatelekeza.
Yul Edochie amekuwa akiangaziwa sana mitandaoni katika muda wa miaka mitatu hivi, baada ya kutangaza kwamba ameoa mke wa pili ambaye ni mwigizaji mwenza Judy Austin.
Mke wake wa kwanza alipinga vikali hatua hiyo akisema hayuko tayari kuwa kwenye ndoa ya wake wengi.