Ykee Benda amchumbia mpenzi wake Emilly

Hatua hii inajiri baada ya kuvunjika kwa uhusiano kati yake na mama ya mtoto wake Julie Batenga.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki nchini Uganda na mmiliki wa kampuni ya Mpaka Records, Ykee Benda, sasa ameondoka rasmi kwenye soko la mahusiano na ndoa baada ya kumvisha pete ya uchumba mpenzi wake, Emilly, katika sherehe ya kupendeza iliyoandaliwa katika Divine Resort.

Mwimbaji huyo wa kibao maarufu ‘Farmer’ alipiga goti chini ya upinde mkubwa wa maua uliokuwa na umbo la moyo, uliopambwa kwa maua meupe na ishara iliyokuwa na maneno ‘WILL YOU MARRY ME?’ na Emilly akakubali ombi hilo.

Ilikuwa hafla ya faragha ya kifahari lakini ilivutia hisia za mashabiki wengi, huku picha na video zikisambaa kwa kasi mitandaoni.

Watu maarufu na mashabiki wamewatumia wapenzi hao jumbe za pongezi, wakisherehekea hatua hiyo ya kimapenzi ya kishujaa kutoka kwa nyota huyo.

Uchumba huu unaashiria mwanzo mpya kwa msanii huyo wa umri wa miaka 32, ambaye hivi karibuni alifichua kuwa alikuwa na mipango ya kufanikisha ndoa mwaka 2025.

Akizungumza mwaka jana, Ykee Benda alielezea hamu yake ya kukua binafsi sambamba na taaluma yake inayozidi kuimarika katika muziki. “Kufunga ndoa ni jambo muhimu pia” alisema wakati huo akiongeza kusema kwamba katika maisha, mtu anahitaji mtu wa kuwa naye hadi uzee. Jambo alilotaja kuwa la msingi sana.

Kwa kweli, kwa kumvisha pete Emilly, msanii huyo ameonyesha dhamira ya dhati ya kujenga uhusiano wa kudumu na wenye maana.

Baada ya kuvunjika kwa uhusiano wake wa awali uliovuma na mama ya mtoto wake Dante aitwaye Julie Batenga, Ykee Benda sasa ameonekana kuchukua mwelekeo mpya wa mapenzi wenye misingi ya uaminifu na ukweli.

Share This Article