Yiwu: Mji wa China unaovutia mamilioni ya wafanyabiashara kutoka kote duniani

Martin Mwanje
4 Min Read
Soko la Biashara ya Kimataifa la Yiwu linalopatikana nchini China

Ni majira ya saa 3:50 usiku ninapoabiri ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Guangzhou Baiyun, nikiwa safarini kuelekea mjini Yiwu.

Unapotalii kila pembe ya dunia, utabaini kuwa mji wa Yiwu umejizolea sifa sufufu kama kitovu cha biashara ya bidhaa ndogondogo.

Ni mji ambao unapatikana katika mkoa wa Zhejiang, kusini mashariki mwa China.

Ndegeni, nachukua muda kutupa macho huku na kule yamkini kutabiri utayari wa ndege kuondoka baada ya kuelemewa na safari ndefu yenye uchovu mwingi.

Ni wakati huo macho yangu yanapokutana na makumi ya raia kutoka mataifa mbalimbali.

Sura na lafudhi zao zinanishtakia baadhi wametokea nchi kama vile Nigeria, India, Pakistan, Tanzania na Burundi.

Pembeni yangu, aliketi binti mmoja aliyeonekana mwenye shughuli nyingi kwenye simu yake ya mkononi.

Awali, nilimsikia akizungumza lugha ya Kiswahili. Maongezi yake yakafanya kazi ya kutambua alikotoka kuwa rahisi mno kupitiliza.

“Nairobi vipi? Na biashara Gikomba ilikuwaje leo? Punde nikimalizana na mambo ya mzigo wangu Yiwu nitarejea,” binti yule alimwambia mwenzake upande wa pili.

Wakati wa mazungumzo marefu kati yake nami, nikasadiki kuwa hakika raia wengi wa kigeni walioabiri ndege hiyo walikuwa wafanyabiashara.

Ghafla, kiu yangu ya kutaka kufahamu mengi zaidi kuhusu mji wa Yiwu iliongezeka.

Punde tulipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Yiwu na kuabiri teksi za kutupeleka hotelini ili tukapumzike, uzoefu wa raia hao wa kigeni kuzungumza na madereva, baadhi katika lugha ya Kichina, ulidhihirisha kuwa hakika wao walikaribia kuwa wenyeji wa mji huo.

Soko la Biashara ya Kimataifa la Yiwu

 Keshoye, eneo la kwanza kutembelea katika mji wa Yiwu lilikuwa Soko la Biashara ya Kimataifa la Yiwu.

Kwa kweli, itakuwa sawia na kujidanganya ikiwa utadai kutembelea mji huo bila kufika soko hili, ambalo kwa kawaida hufurika wateja kutoka kila sehemu ya dunia.

Ni soko lenye ukubwa wa mita milioni 6.4 za mraba likiwa na zaidi ya maduka 75,000 yanayouza bidhaa ndogo ndogo zaidi ya milioni 2 kwa wateja mbalimbali kutoka kote duniani.

“Ukubwa wa soko hili unatoshea viwanja 900 vya soka,” ananiambia Tony, Mkenya ambaye ameishi nchini China kwa kipindi cha miaka 10 na kuimaizi lugha ya Kichina utadhani alizaliwa huko katika mji wa Yiwu.

“Nalo limegawanywa katika maeneo matano,” ananielezea zaidi wakati tukitalii eneo la 1 ili kujionea vitu vinavyouzwa huko.

 

 

Hususan, kilichonivutia zaidi kwenye soko hili ni mpangilio wake.

Walioratibu mpangilio huo waliwarahisishia kazi wateja kwani walihakikisha bidhaa fulani zinapatikana katika eneo maalum.

 

Mathalan, ukitaka maua na vinyago, unajua unapaswa kutembelea eneo la 1, mapambo ya vito kama vile pete, mikufu na bangili vikipatikana eneo la 2, wakati vitu vya kutengenezwa kwa mikono kama vile vinyago vikipatikana eneo la 3 na kadhalika.

“Hapa hakuna kupoteza muda. Mteja huja akielekea eneo mahususi kwa sababu anafahamu anachokitaka kinapatikana huko,” ananielezea Tony wakati akinisaidia kununua mwanasesere.

Isitoshe, bidhaa zenyewe zinapatikana kwa kiasi kidogo cha fedha, na kwa yuan mia moja pekee, niliweza kujinunulia bidhaa mbalimbali kwa bei nafuu.

Yamkini hii ni kwa sababu bidhaa kwenye soko hilo zinauzwa kwa bei ya rejareja au ya jumla, kitu ambacho kimewavutia wateja wengi tangu kuasisiwa kwa soko hilo.

Mwaka 2024, mapato yaliyotokana na biashara kwenye soko hilo, hususan uuzaji wa bidhaa nje ya China, yalifikia yuan bilioni 80, na usimamizi wa soko hilo ulinitaarifu kuwa unalenga kuhakikisha fedha hizo zinafikia yuan bilioni 100 mwaka huu wa 2025.

Hadi kufikia wakati nikiondoka, sikufanikiwa kutembelea maeneo yote matano ya biashara kwenye soko hilo.

Ila, niliazimia kuwa sawia na wateja niliokuwa nao kwenye ndege, nami nitakuwa mteja wa mara kwa mara kwenye soko hilo wakati nikijribu kutia guu katika nyanja ya biashara.

Share This Article