Yemi Alade afurahikia Kwita Izina nchini Rwanda

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii maarufu wa muziki wa asili ya Nigeria Yemi Alade alifurahikia muda wake nchini Rwanda alipokuwa huko kuhudhuria sherehe ya kuwapa majina sokwe wachanga.

Taifa la Rwanda limekuwa likiendesha hafla hii kila mwaka kwa miaka 20 sasa kwa lengo la kupiga jeki utalii nchini humo.

Alade alichapisha picha zilizoonyesha matukio ya ziara yake katika eneo la Kinigi nchini Rwanda ambapo alifunga safari hadi vilimani, akampata sokwe wa umri wa miezi minne na akampa jina la “Kundwa”.

Kulingana naye, jina Kundwa linamaanisha kupendwa ndiposa akalichagua.

Baadaye alichapisha picha nyingine zilizomwonyesha akihudhuria mkutano rasmi wa sherehe hiyo ambao pia alihutubia akiwa amevaa vazi la kifalme la Rwanda kwa jina “Imishana”.

Alade alikuwa mmoja kati ya wageni mashuhuri wapatao 40 kutoka ndani na nje ya Rwanda waliotunukiwa fursa ya kipekee ya kuwapa sokwe wapatao 100 majina.

Msanii huyo alishirikisha wafuasi wake mitandaoni kwa aliyoyaona nchini Rwanda akisema, “Ilikuwa ni mapenzi ya mara ya kwanza” akirejelea wakati alimtia Kundwa machoni hata kabla ya kumpa jina.

Alieleza undugu wa karibu uliopo kati ya binadamu na sokwe akibainisha kuwa wanashiriki asilimia 96 ya msimbojeni almaarufu DNA pamoja na kipindi sawa cha ujauzito.

“Ni binamu zetu wa mbali” alisema, akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi wanyamapori na kuweka usawa kati ya falme za binadamu na wanyama.

Sherehe ya Kwita Izina, iliyoanzishwa kutokana na tamaduni za Kinyarwanda za kuwapa watoto majina, imefanikiwa kuwapatia majina Sokwe 397 tangu mwaka 2005, ikionyesha dhamira ya Rwanda katika utalii endelevu na wa kuwajibika.

Share This Article