Wizara ya Utalii kushirikiana na kaunti kufufua utalii nchini

Martin Mwanje
2 Min Read

Wizara ya Utalii itashirikiana bega kwa bega na kaunti zote 47 kukuza sekta ya utalii nchini. 

Waziri wa Utalii Rebecca Miano anasema wizara hiyo ina lengo la kuvutia watalii milioni 5 kufikia mwaka 2027.

Kenya kwa sasa inavutia watalii milioni 2.

Anasema hatua hiyo itahusisha kuipigia debe sekta hiyo vilivyo na wadau wote kukusanya rasilimali ili kufikia lengo hilo.

“Tunataka kufanya kazi kwa karibu zaidi na kaunti na wenye hoteli na kubuni mikakati ya kufufua sekta hiyo,” alisema Waziri Miano wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili katika kaunti za Kilifi na Mombasa.

Miano alitoa wito kwa kaunti kutumia nyanja zingine kuvutia watalii kama vile kutembelea wanyamapori na fukwe mara kwa mara pia vyakula.

“Tukipata watalii zaidi, kila mtu ananufaika ikiwa ni pamoja na kubuni nafasi zaidi za ajira kwa ajili ya vijana wetu,” alisema Waziri huyo.

Aliongeza kuwa wizara yake itanadi uwezo wa kaunti katika maonyesho mbalimbali duniani, na kuzitaka kaunti hizo kutayarisha programu za kuzinadi ili kurahisha mpango huo.

“Tunataka kuzinadi kaunti kikanda na kimataifa, wenye hoteli wanapaswa pia kutekeleza wajibu wao kuukuza utalii kufikia kiwango cha ulivyokuwa awali,” alisema Waziri Miano.

Gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Mung’aro aliahidi kuzileta pamoja kaunti za Pwani na kubuni mpango wa pamoja wa kuzinadi kaunti hizo.

Waziri Miano baadaye alienda kushuhudia ujenzi unaoendelea wa Chuo cha Utalii ambacho kinatarajiwa kutoa mafunzo kwa maelfu ya vijana punde kitakapokamilika.

Share This Article