Wizara ya Elimu nchini imeomboleza wanafunzi walioangamia kwenye ajali ya barabarani kwenye barabara ya kutoka Wundanyi kuelekea Mwatate.
Katika taarifa, Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba alisema, “Nimesikitishwa na habari za kuhuzunisha za ajali mbaya iliyotokea Februari Mosi, 2025 kwenye barabara ya Wundanyi-Mwatate iliyosababisha vifo vya watu 6 wakiwemo wanafunzi wanne wa shule ya upili ya wavulana ya Dr. Aggrey.”
Waziri huyo aliendelea kwa kutoa rambirambi zake na za wizara nzima ya elimu kwa familia na marafiki za walioangamia.
“Tunaomba Mungu awape nguvu na ujasiri wakati huu mgumu. Tunaombea waliojeruhiwa afueni ya haraka,” aliandika Waziri Migos huku akimalizia kutakia nyoyo za walioangamia mapumziko ya amani.
Wanafunzi hao walikuwa sehemu ya abiria wa basi moja ambalo lilihusika kwenye ajali baada ya dereva kushindwa kulidhibiti na likaishia kubingiria.
Walikuwa wametumwa nyumbani kufuatia kisa cha moto shuleni ambao uliteketeza bweni moja shuleni humo. Dereva wa basi hilo naye alifariki kwenye ajali hiyo.
Tukio hilo limesababisha mbunge wa eneo la Wundanyi Danson Mwashako aombe mamlaka ya barabara kuu nchini KENHA itekeleze ripoti kuhusu eneo la Josa ambalo hushuhudia ajali nyingi.
Mbunge huyo naye alituma rambi rambi kwa familia za walioangamia kwenye ajali hiyo hasa familia za wanafunzi wa shule ya ulipi ya Dr. Aggrey.