Wizara ya Afya imezindua kampeni ya kitaifa inayolenga kukabiliana na matumizi yanayoongezeka ya mihadarati nchini.
Katibu katika Wizara hiyo Mary Muthoni anasema kampeni hiyo hasa italenga maeneo ambayo yameathiriwa mno na matumizi ya pombe na dawa za kulevya.
“Kampeni hii, itakayotekelezwa katika kaunti zote 47 katika makundi 10, inaangazia kuzipatia jamii maarifa na vifaa vinavyohitajika kuzuia uraibu wa dawa hizo na kusaidia katika kukomesha matumizi ya mihadarati,” alisema Muthoni.
Katibu huyo aliyezungumza wakati wa mkutano wa washikadau uliofanyika jijini Mombasa na uliowaleta pamoja wawakilishi kutoka kaunti sita za Pwani, alisisitiza umuhimu wa hatua za pamoja kukabiliana na matumizi ya mihadarati nchini.
“Vita dhidi ya matumizi ya mihadarati ni kipaumbele cha kitaifa. Tunapaswa kuziwezesha jamii, kuimarisha utekelezaji sheria na kupatiana mifumo thabiti ya usaidizi ili kuvunja mduara wa uraibu huo.”
Kampeni hiyo inakuja wakati ambapo takwimu zinaonyesha Wakenya milioni 4.7 wanatumia mihadarati, ikiwa ni pamoja na pombe na tumbaku.