Wizara ya Afya imesaini mwafaka wa ushirikiano kati yake na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), Shirika la Afya ya Kidijitali, na shirika la kusambaza dawa nchini (KEMSA), katika hatua inayolenga kuboresha utoaji huduma za afya ya kijamii.
Mwafaka huo ambao utashirikisha hospitali za kitaifa na zile za rufaa unalenga kuimarisha utoaji huduma za matibabu.
Hafla ya kusaini kwa makubaliano hayo iliandaliwa Jumanne na kushuhudiwa na Waziri wa Afya Aden Duale, Afisa Mkuu Mtendaji wa KEMSA Dkt. Waqo Ejersa, Afisa Mkuu Mtendaji wa SHA Dkt. Mercy Mwangangi, na Katibu wa Huduma za Matibabu Dkt. Ouma Oluga.
Duale alikariri kujitolea kwa serikali kuimarisha utendakazi wa KEMSA, ili kuhakikisha upatikanaji wa dawa za viwango vya juu katika hospitali za umma.
Aidha, Duale alisema kuwa tayari wizara yake imeanza mkakati wa kutoa shilingi bilioni 1.5, kufadhili shughuli za KEMSA na mkopo mwingine wa shilingi bilioni 10.