Wizara ya Afya yaimarisha vita dhidi ya magonjwa ya Hepatitis na Mpox

Tom Mathinji
2 Min Read

Wizara ya Afya imeimarisha juhudi zake za kukabiliana na msambao wa ugonjwa wa Hepatitis na Mpox kote nchini, ikitaja ongezeko la maabukizi ya magonjwa hayo na ukosefu wa uhamasisho kwa umma kama changamoto kuu.

Akizungumza jijini Mombasa wakati wa sherehe ya kuadhimisha siku ya Hepatitis Duniani, Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dkt. Patrick Amoth, alisema takriban asilimia tatu ya Wakenya wanaishi na ugonjwa wa Hepatitis B na C, huku wengi wao wakikosa kutibiwa kutokana na ukosefu wa ufahamu hasa katika maeneo ya mashinani.

“Serikali inagharimia matibabu ya ugonjwa wa Hepatitis B na C, kwa hivyo wagonjwa watatibiwa bila malipo,’ alisema Dkt. Amoth.

Aliongeza kuwa hatua hiyo inatarajiwa kusaidia katika utambuzi wa mapema wa ugonjwa huo na usimamizi wake.

Dkt. Amoth alisema chini ya ajenda ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, Wizara ya Afya inafanya kazi kugatua vipimo na huduma za matibabu, hasa katika maeneo yanayoathiriwa zaidi na ugonjwa huo na yasiyojiweza.

Kuhusiana na ugonjwa wa Mpox, Dkt. Amoth alithibitisha maambukizi 300 kote nchini huku visa 138 na vifo vifo 5 vikiripotiwa katika kaunti ya Mombasa.

Amesema Wizara inafanya kazi bega kwa bega na serikali ya kaunti ya Mombasa kuongeza hamasa ya umma, kuongeza vipimo na kuhakikisha wagonjwa waliothibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo wanafuatiliwa kwa karibu na kupata huduma za matibabu kwa wakati mwafaka.

Share This Article