Wizara ya Afya yaimarisha juhudi za kuboresha mpango wa UHC

Wizara hiyo inatumia uvumbuzi wa kidijitali katika kuimarisha usambazaji wa huduma za afya kwa wote kote nchini.

Marion Bosire
2 Min Read

Wizara ya Afya imeimarisha juhudi za kuimarisha mpango wa upatikanaji wa huduma sawa za afya kwa wote, UHC kupitia Mamlaka ya afya ya jamii (SHA) kupitia uvumbuzi wa kidijitali.

Uvumbuzi huo wa kidijitali unalenga kulainisha huduma za afya kote nchini.

Akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya kila wiki leo, Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dkt. Patrick Amoth aliangazia kuanzishwa kwa vipengele muhimu vinayolenga kuboresha mfumo wa huduma za afya.

Hatua moja kuu ni utekelezaji wa mfumo wa kina na jumuishi wa habari kuhusu afya, ambao umepiga hatua kubwa.

Mfumo huo unajumuisha ubadilishanaji wa habari za kiafya, unaoendelea pamoja na sajili za wateja, watoaji huduma na vituo vya afya.

Mfumo huo mpya unatarajiwa kuanza kufanya kazi kikamilifu kufikia Disemba 2025.

Vile vile Wizara ya Afya imesambaza mfumo wa Taifa Care kwenye taasisi za afya kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa habari kuhusu hospitali mbali mbali.

Ili kuwapa wananchi uwezo zaidi, wizara hiyo imezindua programu ya kidijitali kwa jina ‘Afyangu’ ambayo inawezesha mtu kujisajili kwenye SHA na kuweza kusimamia mipango yake ya kiafya kwa urahisi.

Uvumbuzi huu unawakilisha hatua muhimu katika kuimarisha utoaji huduma, uwazi na ufanisi katika sekta ya afya, na hivyo kutoa fursa kwa upatikanaji bora wa huduma za afya kwa wote.

Share This Article