Wizara ya afya kuondoa kesi dhidi ya Grace Njoki

Tom Mathinji
2 Min Read
Wizara ya afya kuondoa kesi dhidi ya Grace Njoki.

Katibu wa idara ya huduma za matibabu Harry Kimtai, alikuwa na wakati mgumu siku ya Alhamisi kuelezea wabunge sababu za kutiwa nguvuni kwa Grace Njoki mwenye umri wa miaka 61, aliyeingia kwa njia tatanishi katika jumba la afya juma lililopita.

Wakati wa mkutano wa wabunge mjini Naivasha, wabunge hao walimshinikiza Kimtai kuelezea makosa ambayo Njoki alitekeleza alipozuru makao makuu ya wizara ya afya kuwasilisha malalamishi yake kuhusu halmashauri ya afya ya jamii SHA.

Kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah, alihoji ni kwanini serikali imemshtaki Njoki, akitaka kufahamishwa ni nani mlalamishi wa kesi hiyo.

“Tunataka kufahamu mambo matatu. kwanza ni nani mlalamishi aliyesababisha Njoki kutiwa nguvuni? Ni SHA?, ni wizara ya afya? au ni maafisa wa polisi waliotekeleza hatua hiyo bila uchunguzi? Tunataka kufahamishwa makosa ya Njoki,” aliuliza Ichung’wah.

“Tuliona kwenye magazeti kwamba ameachiliwa kwa dhamana ya polisi ya shilingi 50,000. ikiwa wewe ndiwe mlalamishi, je umeondoa kesi hiyo? au kuna kola la jinai mnalofuata dhidi Njoki?,” aliongeza mbunge huyo wa Kikuyu.

Katika majibu yake, Kimtai alithibitisha kuwa mlalamishi katika kesi hiyo ni wizara ya afya, akisema ameshtakiwa kwa kuingia kwenye jengo hilo bila idhini na kuzua vurugu, maelezo ambayo yalipokewa kwa makelele na baadhi ya wabunge wanawake.

Njoki alitiwa nguvuni katika hospitali moja Jijini Nairobi alipokuwa akitafuta matibabu, na kufunguliwa mashtaka ya kuzua vurugu katika afisi za wizara ya afya.

Kufuatia shinikizo kali, katibu Kimtai aliwahakikishia wabunge hao kuwa wizara ya afya itaondoa kesi hiyo dhidi ya Njoki.

Hatua ya kukamatwa kwa Njoki, ilikashifiwa vikali, huku wito ukitolewa wa kuachiliwa kwake.

TAGGED:
Share This Article