Willy Paul akanusha madai ya kuuza muziki wake

Marion Bosire
1 Min Read

Willy Paul au ukipenda Willy Pozee amekanusha madai kwamba aliuza hakimiliki za muziki wake wote na akatumia pesa alizopata vibaya.

Mwanamuziki huyo alikanusha madai hayo kwenye video aliyochapisha kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii ambapo alisema uvumi huo umechochewa na maisha ya hali ya juu anayoishi.

“Nimeona kuna watu ukiishi maisha mazuri katika nchi hii, inawauma ni kama inawazuia kuishi maisha yao.” alisema mwanamuziki huyo akiongeza kwamba hajauza muziki wake.

Alijitetea akisema kwamba yeye ni msanii ambaye amejipanga anamiliki biashara ambazo zinafanya vyema ndiposa anaweza kuishi maisha hayo mazuri.

Haya yanajiri baada ya mchanganuzi wa masuala ya burudani, wasanii na watu maarufu mitandaoni anayejiita Sanato Sauti ya Ground, kudai kwamba Pozee aliuza muziki wake wote.

Sabato alidai pia kwamba msanii huyo alitumia pesa hizo visivyo akiwa na wanawake, madai yaliyomkera Willy Paul ambaye aliamua kujibu kwa nia ya video.

Pozee amesema kwamba hatabadili mtindo wake wa maisha na kamwe hataacha muziki hadi siku ambayo yeye mwenyewe ataamua kuuacha.

Ametangaza pia ujio wa wimbo wake mpya kwa jina Ngunga ambao amewahusisha Patelo na Dee.

Share This Article