Bunge la Taifa halijawafadhili wabunge 100 kwenda jijini Addis Ababa nchini Ethiopia kumuunga mkono Raila Odinga kugombea uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Kumekuwa na madai kuwa bunge hilo limefadhili wabunge wasiopungua 100 kwenda Addis Ababa kumshabikia Raila wakati akitafuta kumrithi mwenyekiti wa AUC anayeondoka Moussa Faki.
Katika taarifa yake kwa bunge hilo leo Alhamisi, Spika Moses Wetang’ula amebainisha kuwa kwa mujibu wa kanuni za bunge, amepokea karibu notisi 40 za wabunge wanaodhamiria kusafiri.
Amesema wabunge hao watasafiri kwa gharama zao wenyewe ili kwenda kumuunga mkono Raila.
“Ujumbe rasmi wa bunge unajumuisha wabunge wanne pekee. Wabunge wengine 40 watasafiri katika nyadhifa zao za kibinafsi kama raia na viongozi, na kugharamia matumizi yao wenyewe. Tunawapongeza kwa kuchukua wajibu huu wa kizalendo,” aliongeza Wetang’ula.
Uchaguzi wa kumchagua mwenyekiti mpya wa AUC utaandaliwa Jumamosi hii ambapo viongozi wa nchi mbalimbali za Afrika watapiga kura.
Raila atamenyana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Madagascar Richard Randriamandrato.
Mgombea huyo wa Kenya ameelezea matumaini kuwa atautwaa wadhifa huo hasa baada ya kufanya kampeni kali ambapo alitembelea mataifa mbalimbali ya Afrika kujinadi kwa viongozi wa nchi hizo.
Jana Jumatano, Raila alikuwa mjini Bujumbura kutafuta uungwaji mkono kabla ya kuelekea Addis Ababa.