Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula leo Jumatano atatoa mwelekeo kuhusu ni mrengo upi baina ya Azimio na ule wa Kenya Kwanza ulio wabunge wengi katika bunge hilo.
Hii inafuatia babe ulioshuhudiwa katika bunge hilo na lile la Seneti, wakati wanachama wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya walichukua nafasi za walio wengi katika mabunge yote mawili kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu.
Hata hivyo, Wetang’ula anasisitza kuwa mahakama haina mamlaka ya kutangaza mrengo ulio na wabunge wengi au wachache bungeni, akisema kuwa jukumu hilo ni la bunge.
Wetang’ula tayari amekataa wito wa kumtaka aondoke na kumwachia Naibu wake Gladys Boss Shollei wadhifa wake, kufuatia uamuzi wa mahakama uliotilia shaka uwezo wake wa kuwa mwamuzi asiyeegemea upande wowote.
Kikao cha Bunge la Taifa kilisitishwa kwa muda baada ya baadhi ya wabunge wa Azimio kumzuia Naibu kiongozi wa wengi Owen Baya kuwasilisha taarifa bungeni jinsi inavyohitajika na kanuni za bunge.
Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo alimtaka Wetang’ula kuondoka wadhifani na kumpisha Naibu wake Gladys Shollei kuchukua wadhifa wa spika kufuatia uamuzi huo wa mahakama.
Macho yote sasa yameelekezwa kwa Maspika wa mabunge yote mawili kutoa mwelekeo kuhusu uamuzi huo wa Mahakama Kuu.