Bunge la Taifa la Kenya limetoa ahadi ya kuimarisha uhusiano wake na Somalia kupitia mipango ya kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa bunge la Somalia.
Hatua hiyo inaimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili jirani.
Tangazo hilo lilitolewa na Spika wa Bunge la Taifa la Kenya Moses Wetang’ula baada ya kuwa mwenyeji wa balozi wa jamhuri ya Somalia Jabril Ibrahim Abdulle.
Balozi huyo na ujumbe wake walimtembelea Wetang’ula kuwasilisha ujumbe wa heri njema kutoka kwa Spika wa Bunge la Somalia Sheikh Adan Mohamed Nur (Madobe).
Wetang’ula alithibitisha kujitolea kwa Kenya kupiga jeki bunge la Somalia kuafikia ukuaji na maendeleo.
“Kenya iko tayari kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa bunge la Somalia kupitia taasisi zetu na mipango ya kujifahamisha,” alisema Wetang’ula.
Wetang’ula aliongeza kuwa wafanyakazi wa Bunge la Somalia watajumuishwa kwenye kamati za bunge la Kenya ili wapate ujuzi wa kazi.