Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula ameitaka jamii ya Abagusii kujiepusha na siasa za kikabila anazosema zimepitwa na wakati.
Amesema siasa kama hizo zina hatari ya kuitenganisha jamii hiyo na Wakenya wengine.
Akizungumza leo Alhamisi wakati wa mkutano wa uwezeshaji wanawake uliofanyika katika wadi ya Bugusero, eneo bunge la Kitutu Chache Kusini, kaunti ya Kisii, Wetang’ula amewataka wakazi kukumbatia umoja na ujumuishaji, hata ikiwa baadhi ya wanasiasa kutoka eneo hilo wametangaza azima ya kugombea urais.
Waziri wa zamani wa Usalama wa Taifa Dkt. Fred Matiang’i na Jaji Mkuu mstaafu David Maraga ni wanasiasa wawili kutoka eneo la Kisii waliotangaza rasmi nia yao ya kumbandua madarakani Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.
Isitoshe, ripoti zinaashiria kuwa Dkt. Matiang’i kesho Ijumaa atapokezwa kijiti cha kuwania urais kwa tiketi ya chama cha Jubilee kwenye uchaguzi mkuu wa 2027.
“Nataka kuiomba jamii ya Abagusii kutonaswa kwenye mtengo wa kujitenga na Wakenya wengine. Siasa za aina hiyo hazina nafasi katika Kenya ya sasa,” alionya Wetang’ula.
Spika akitumia fursa hiyo kumsuta mbunge wa eneo bunge la Kitutu Chache Kusini Anthony Kibagendi kwa kumkosea heshima Rais Ruto.
Kibagendi ni mkosoaji mkubwa wa Rais Ruto na amekuwa mstari wa mbele kumshabikia Dkt. Matiang’i kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.