Wendy Williams asherehekea siku ya kuzaliwa

Alijiunga na watu wake wa karibu wakiwemo waliofanya kazi naye awali kwa chakula cha jioni jijini New York.

Marion Bosire
2 Min Read

Wendy Williams alisherehekea siku yake ya kuzaliwa Ijumaa Julai 18, 2025 na marafiki jijini New York alipokuwa akitimiza umri wa miaka 61.

Mtangazaji huyo wa awali wa runinga alionekana mwenye furaha huku akitabasamu akiwa na watu wake wa karibu katika hoteli ya Tucci kwa chakula cha jioni.

Video iliyosambazwa mitandaoni iliyonakiliwa wakati alikuwa akielekea eneo la sherehe, ilimwonyesha akisema kwamba kila kitu kilikuwa kinaendelea kwa njia shwari.

Williams alikuwa amevaa nguo fupi yenye madoadoa ya chui, viatu vya wanamichezo vya rangi nyeupe na begi kubwa ya rangi nyeusi. Uso wake nao ulikuwa umepodolewa na alikuwa amevaa miwani.

Picha zilizochapishwa rafiki ya Wendy, Brendan Higgins, zilionyesha kwamba mtangazaji huyo alikuwa pamoja na aliyekuwa mtayarishaji wa kipindi chake Suzanne Bass, mpwa wake na mwongoza kipindi cha asubuhi cha ABC Miami Alex Finnie kati ya wengine.

Akizungumza na mwanahabari mapema wiki iliyopita, Wendy alisema kwamba kitu ambacho anataka sana kwa sasa ni kukomeshwa kwa usimamizi wa kisheria aliowekewa.

Wendy anataka kuwa huru kutokana na usimamizi huo wenye utata ulioanza Mei 2022 na mara kwa mara ameonyesha kutoridhishwa na vitendo vya wale waliotwikwa jukumu la kufanya maamuzi kuhusu maisha yake.

Mtangazaji huyo anasema anahisi kwamba yeye ni mfungwa katika makazi aliyowekwa kwa lazima kwani anaishi na wagonjwa wakongwe ambao anasema maradhi yao ni sugu na yeye yuko sawa.

Share This Article