Waziri wa zamani Joseph Munyao afariki

Tom Mathinji
1 Min Read
Aliyekuwa waziri Joseph Munyao amefariki.

Waziri wa zamani Joseph Konzolo Munyao ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 85.

Munyao ambaye alikuwa mbunge wa muda mrefu wa eneo bunge la Mbooni, alifariki siku ya Jumamosi, Novemba 22, 2025 akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi.

Akituma rambirambi kwa jamaa na marafiki wa Munyao, Rais William Ruto alimtaja kiongozi huyo, kuwa ambaye aliwahudumia wananchi kwa uadilifu wa hali ya juu.

“Tumehuzunishwa na kifo cha Joseph Munyao, ambaye pia ni mbunge wa zamani wa eneo bunge la Mbooni, kaunti ya Makueni,” aliomboleza Rais Ruto kupitia ukurasa wake wa X.

Rais alisema Munyao alishirikiana kwa karibu na wakulima kuimarisha hali yao ya maisha.

“Utumishi wake kwa umma uliashiria kujitolea kwake, ambako kuliboresha maisha ya wengi.”

Ruto aliitakia familia ya Munyao faraja kwa kutambua kuwa urithi wake utasalia katika jamii aliyoitumikia na kumwomba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema.

Share This Article