Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku amesisitiza umuhimu wa watumishi wa umma nchini Kenya kudumisha viwango vya juu vya taaluma na uadilifu kazini. Amewataka maafisa wote wa serikali kufika kazini mapema, kuwahudumia Wakenya kwa heshima na utu, na kuepuka vitendo vyovyote vya rushwa na uzembe kazini.
“Watumishi wa umma wanapaswa kukwepa rushwa na uvivu. Serikali haitavumilia aina yoyote ya maovu katika utumishi wa umma,” alisema Waziri Ruku, na kuongeza kuwa serikali ya Rais William Ruto imejizatiti kuunda mfumo wa utumishi wa umma unaojali na unaofanya kazi kwa ufanisi.
“Rais amenikabidhi jukumu la kuhakikisha tunaunda utumishi wa umma unaowajibika kwa wananchi wote bila kujali asili yao.”
Akizungumzia siasa, Ruku alipuuzilia mbali juhudi za upinzani za kuigawa nchi kwa misingi ya kikabila. Alisisitiza dhamira ya serikali ya kuendeleza umoja wa kitaifa, akisema kuwa Kenya ni taifa moja lenye bendera moja, wimbo wa taifa mmoja, na mipaka ya pamoja.
“Hakuna binamu katika nchi hii—sisi sote ni ndugu na dada. Kila Mkenya ana haki ya kuishi na kufanya kazi mahali popote nchini. Kueni macho dhidi ya wanaochochea chuki, maandamano, na uharibifu wa mali ya umma na binafsi,” alionya.
Aidha, alitangaza kuwa serikali inapanga kuajiri walimu wapya 24,000 ifikapo mwezi Januari mwaka ujao, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha elimu kote nchini.
Akizungumza wakati wa ziara ya kuwafariji waathiriwa wa moto katika maeneo ya Gatero na Muthengera, eneo bunge la Laikipia Magharibi, Waziri alidokeza kuwa miradi kadhaa ya uboreshaji wa barabara itatekelezwa katika eneo hilo. Pia alisema kuwa kaya zaidi zitanufaika na mpango wa usambazaji wa umeme wa Last Mile.
Pia alibainisha kuwa hali ya amani na usalama imerejea katika kaunti ya Laikipia baada ya kuajiriwa kwa askari wa akiba 610. Alisisitiza kuwa serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuwapatia vijana ajira, akisema kuwa zaidi ya vijana 400,000 wa Kenya wanafanya kazi katika nchi za kigeni huku wengine wengi wakihusishwa katika mpango wa nyumba za gharama nafuu na kazi za mabadiliko ya tabia nchi (zamani Kazi Mtaani) kote nchini.
Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Laikipia, Jane Kagiri, alipinga vikali mipango ya kuondoa maeneo yoyote ya Laikipia, yakiwemo Nyahururu, kutoka orodha ya maeneo magumu ya kufanyia kazi. Alisema kuwa watumishi wengi wa umma walioko Nyahururu huhudumu maeneo ya mbali, hivyo wanastahili kuendelea kupata marupurupu ya mazingira magumu.

Kagiri alisifu kurejea kwa amani na usalama katika eneo la Laikipia na kutoa wito kwa vyombo vya habari kuangazia mabadiliko hayo chanya ili kuwavutia wawekezaji.
“Laikipia imepiga hatua kubwa katika suala la usalama. Ni wakati wa vyombo vya habari kubadilisha taswira na kuonyesha kuwa sasa hapa ni mahali salama na penye matumaini ya kuwekeza,” alisema.
Mbunge wa Laikipia Magharibi, Wachira Karani, pamoja na Kagiri waliyeandaa ziara hiyo, walieleza kuunga mkono juhudi za maendeleo na misaada kwa wakazi wa eneo bunge hilo.
Walieleza utayari wao wa kushirikiana na serikali kuu kuhakikisha kuwa wakazi wa Laikipia Magharibi na kaunti kwa ujumla wanapata manufaa kutoka kwa mipango ya serikali ya sasa na ya baadaye.
Mbunge wa Kabete, Githua Wamacukuru, aliyeandamana na ujumbe huo, alihimiza wananchi kuendelea kuiunga mkono serikali ya Kenya Kwanza, akitaja mafanikio katika miradi ya barabara, masoko na mipango ya basari. Alitetea juhudi za serikali za kugawa chakula kwa wanaokihitaji na kuwakosoa wale wanaopinga bila kutoa mbadala bora.
