Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku leo Ijumaa alifanya ziara za kushtukiza katika vituo vya Huduma Centre jijini Nairobi.
Vituo hivyo hutumiwa mno na Wakenya wanaotafuta huduma mbalimbali kama vile kupatiwa vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho vya kitaifa na leseni za udereva.
Ruku alifanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha Huduma Centre kilichopo kwenye jengo la GPO na kile kilichopo mtaani Eastleigh.
Ziara hizo ni sehemu za kukagua kiwango cha huduma zinazotolewa kwa raia na kuangazia mapungufu wanayokumbana nayo wafanyakazi wa vituo hivyo kwa lengo la kuyatafutia ufumbuzi.
Wakati ziara zake za leo Ijumaa, Ruku aliwapongeza wafanyakazi kutokana na uanataaluma wao, uimara na uvumbuzi katika utoaji huduma muhimu licha ya kufanya kazi kwa kutumia rasilimali chache zilizopo.
“Nimefurahishwa na kiwango cha uanataaluma na kazi inayofanywa ambayo nimeshuhudia leo. Inatia moyo kuona watumishi wa umma wakifjituma zaidi licha ya rasilimali chache walizonazo, kuonyesha kuwa wamejitolea kuwahudumia Wakenya,” alisema Waziri huyo alipotembelea kituo cha Huduma Centre mtaani Eastleigh.