Waziri Oparanya bado ana kesi ya ufisadi ya kujibu

Waziri huyo wa Vyama vya Ushirika anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi ya kima cha shilingi milioni 56.7 na matumizi mabaya ya mamlaka alipohudumu kama Gavana wa Kakamega.

Martin Mwanje
2 Min Read
Wycliffe Oparanya - Waziri wa Vyama vya Ushirika

Mahakama Kuu jijini Nairobi imebatilisha uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga koundoa mashtaka ya ufisadi dhidi ya Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya.

Oparanya alikabiliwa na mashtaka ya ufisadi ya kima cha shilingi milioni 56.7 kutoka kwa wakurugenzi wa kampuni ya Sabema International Limited na ile ya Sesela Resources Limited wakati alipohudumu kama Gavana wa Kakamega.

EACC ikisema Oparanya alitumia fedha hizo kujilimbikizia mali katika mtaa wa kifahari wa Karen.

Aidha, Oparanya alikabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya mamlaka wakati wa utawala wake, mashtaka ambayo pia yaliondolewa na DPP kabla ya Oparanya kuteuliwa kuwa Waziri serikalini.

Hata hivyo kwenye uamuzi wake, mahakama imetaja hatua ya kuondoa mashtaka dhidi ya Gavana huyo wa zamani wa Kakamega kuwa isiyokuwa ya kikatiba.

Mahakama ikisema DPP ilichukua uamuzi huo bila uwazi na kushauriana na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na kwa misingi hiyo kuingilia mamlaka ya uchugunzi ya tume hiyo.

Ifahamike kwamba EACC siku chache zilizopita ilituhumu DPP kutokana na hulka yake ya kuondoa mashtaka dhidi ya washtakiwa bila kutafuta ushauri wake.

Licha ya uamuzi wake, mahakama iliepuka kutoa agizo la kutengua uteuzi wa Oparanya kama Waziri katika serikali jumuishi.

Kesi dhidi ya Oparanya sasa itaendelea huku hatima yake kama Waziri wa Vyama vya Ushirika ikiwa sasa haijulikani.

Hatua ya mahakama inakuja wakati ambapo Rais William Ruto ameahidi kukabiliana na jinamizi la ufisadi bila kujali hadhi ya wahusika wa uovu huo.

Kiasi kwamba siku chache zilizopita, Ruto alibuni jopo lililozileta pamoja asasi mbalimbali ikiwemo EACC na DPP ili kutafuta mbinu za kuangamiza ufisadi nchini.

Mahakama ilipiga breki utenda kazi wa jopo hilo baada ya kuwasilishwa kwa kesi ya kupinga uhalali wa jopo hilo.

 

 

Share This Article