Waziri wa Leba na Ulinzi wa Jamii, Dkt. Alfred Mutua, ameongoza mkutano wa viongozi kutoka eneo la Ukambani kujadiliana kuhusu nafasi yao katika kutekeleza ajenda ya serikali ya Kenya Kwanza chini ya uongozi wa Rais William Ruto.
Dkt. Mutua alisisitiza umuhumi wa viongozi wa jamii hiyo ya Wakamba kuwa na umoja katika harakati za kutafuta suluhu kwa changamoto zinazokabili eneo hilo.
Viongozi waliohudhuria mkutano huo walikubaliana kwa kauli moja haja ya kuhsirikiana kuhakikisha jamii hiyo inajumuishwa kikamilifu katika maendeleo ya serikali.
Katika kupiga jeki ajenda ya jamii hiyo, viongozi waliohudhuria kikao hicho waliafikiana kuwatembelea wananchi katika kaunti za Machakos, Makueni, na Kitui na pia maeneop yaliyo na idadi kubwa ya jamii ya Wakamba katika kaunti za Nairobi, Mombasa, Kilifi, Taveta, Embu, na Kwale.
Mikutano hiyo na wananchi itawezesha viongozi kufanya maamuzi yafaayo katika kupigania mgao wa maendeleo kutoka kwa serikali.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni pamaja na Wabunge Mwengi Mutuse wa Kibwezi Magharibi, mwenzake wa Machakos Town Caleb Mule, Seneta mteule Beth Syengo, na mbunge Joshua Mwalyo wa Masinga pamoja na wawakilishi wadi kadhaa pamoja na wasomi.