Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amepongeza mpango wa Marekani kuhusu Gaza akisema kwamba Marekani na Israel zina mkakati sawa kuhusu mustakabali wa Gaza.
Netanyahu alisema hayo baada ya mkutano na waziri wa masuala ya kigeni wa Marekani Marco Rubio jijini Jerusalem Jumapili.
Alisema atashirikiana na Marekani kuhakikisha kwamba mpango wa Rais Donald Trump wa kuondoa wapalestina katika eneo la Gaza na kulijenga upya unafanikiwa.
Huku haya yakijiri, Umoja wa Mataifa umeonya kwamba ufurushaji wa lazima wa raia kutoka eneo wanalokalia na kumiliki haukubaliki kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Rubio alisema kwamba mpango wa Trump huenda ulishangaza wengi lakini iligharimu ujasiri kupendekeza suluhisho mbadala kwa mawazo ya zamani.
Netanyahu alisema yeye na Rubio walijadiliana kuhusu namna bora ya kutekeleza mpango wa Rais Trump.
Kuhusu mpango unaoendelea wa kusitisha vita na kubadilishana wafungwa na Hamas, Netanyahu alionya kwamba “malango ya kuzimu” yatafunguliwa iwapo raia wote wa Israel hawataachiliwa.
Rubio kwa upande wake alisema kwamba kundi la wapiganaji la Hamas haliwezi kuendelea kutekeleza shughuli kama jeshi la serikali.
Kulingana naye iwapo hilo litakubaliwa, basi amani haitapatikana.