Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba amekiri kwamba mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu uliozinduliwa mwaka jana haujaafikia matokeo yaliyotarajiwa.
Akizungumza baada ya mkutano na kamati ya kitaifa ya kuhakiki mfumo huo, Ogamba alisema kwamba wizara iliamua kuwa sehemu ya suluhisho na sio sehemu ya tatizo lililopo ndiposa kamati hiyo ikabuniwa.
Ogamba alihakikishia washikadau kujitolea kwa serikali huku akiomba vyuo vikuu kusajili wanafunzi wote hata ingawa mfumo huo wa ufadhili unakumbwa na matatizo.
Mkanganyiko uliopo kuhusu mfumo huo wa ufadhili wa elimu ya juu kulingana na Migos unatokana na ripoti za vyombo vya habari ambazo zinatokana na watu wasio wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma.
Kuhusu ukosefu wa fedha unaokumba taasisi nyingi za elimu ya juu, waziri alifafanua kwamba taasisi zipatazo 23 zinakumbwa na ufilisi.
Alisema kila kisa kama kile cha chuo kikuu cha Moi kinashughulikiwa kivyake.
Mkutano huo uliangazia pia mgomo wa wahadhiri wa vyuo vikuu ambapo Ogamba alidhihirisha matumaini kwamba suluhisho litaafikiwa karibuni.
Waziri Ogamba aliahidi kushughulikia malalamishi ya wanafunzi na kuimarisha uwazi na upatikanaji wa nyaraka muhimu.
Wanafunzi pia watapokea pesa za matumizi huku kamati hiyo ikiongezewa muda hadi itakaposhughulikia kikamilifu matatizo yote.
“Wizara ya elimu imejitolea kuhakikisha mfumo wa ufadhili wa elimu ya juu unafanikiwa katika taasisi zote na kwa wanafunzi wote.” alisema Waziri.
Majadiliano ya jopo hilo na wadau mbali mbali yanatarajiwa kufanikisha uimarishaji wa mfumo huo wa ufadhili kwa manufaa ya wanafunzi na taasisi zote za elimu ya juu nchini.