Waziri wa Utalii na Wanyamapori Rebecca Miano amewahimiza vijana kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara zinazotolewa na serikali, akisisitiza kuwa ujasiriamali ndio njia mwafaka katika soko la ajira linalozidi kuwa finyu.
Akizungumza katika kongamano la biashara lililofanyika mjini Nyahururu, Waziri Miano alieleza kuwa serikali imejitolea kwa dhati kuwasaidia vijana kupitia mipango kama vile Upatikanaji wa Fursa za Ununuzi za Serikali (AGPO) unaowalenga vijana, wanawake, na walemavu.
“Kwa sababu soko la ajira linazidi kupungua, ujasiriamali ndio suluhisho—hasa kwa vijana. Kinachohitajika ni ujasiri, ujuzi, na kujiamini kuanzisha biashara,” alisema Waziri Miano.
Aliongeza kuwa ajira rasmi si ya uhakika tena, na hata inapopatikana, mara nyingi haikidhi matarajio ya vijana wengi. Badala yake, aliwahimiza vijana kujiajiri kwa kuanzisha biashara, wakitumia msaada unaotolewa na serikali.
Miano pia alieleza kuwa serikali imeweka kipaumbele katika kuhakikisha kuwa vijana wanaopania kuanzisha biashara wanapata mitaji ya kuanzia. Alitaja taasisi kama vile Shirika la Maendeleo nchini Kenya (KDC), Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, na taasisi zingine za kifedha zinazotoa mikopo na msaada wa kiufundi kwa wajasiriamali chipukizi.
Aidha, aliwahimiza vijana kutumia taasisi za kukuza uwezo kama vile Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Kiviwanda nchini Kenya (KIRDI) ambayo huwasaidia kwa kutoa huduma za kukuza mawazo ya kibiashara, mafunzo ya kiufundi na mpango wa kulea biashara changa.
“Vijana wana ubunifu, wanafahamu teknolojia, na wana nguvu. Wanaweza kutumia fursa katika sekta za kiteknolojia kama vile eco-tourism, virtual reality, na huduma za kidijitali ambazo zinaweza kuwafikia wateja duniani kote,” aliongeza.
Kongamano hilo, lililoandaliwa na Mhandisi John Ndaiga, liliwaleta pamoja zaidi ya biashara 40 kutoka mji wa Nyahururu na maeneo jirani.
Katika hafla hiyo, Waziri Miano alizindua rasmi kinyozi na spa inayomilikiwa na kijana mjasiriamali, ishara ya wazi kuwa serikali inaunga mkono biashara zinazoendeshwa na vijana.

Kwa upande wake, Naibu Gavana wa kaunti ya Laikipia, Reuben Kamuri, alimpongeza Mhandisi Ndaiga kwa kuajiri zaidi ya vijana kumi katika kinyozi chake. Alisema biashara hiyo si ya kawaida tu, bali imepangwa kwa viwango vya juu na kuwa mfano wa kuigwa.
“Hii si biashara tu—ni biashara ya aina yake,” alisema Kamuri.
“Ninaamini katika kuwaunga mkono vijana kwa sababu wao ndio nguzo ya maendeleo ya uchumi wetu. Nawahimiza vijana kutumia fursa ya asilimia 30 ya zabuni katika serikali ya kaunti ambazo zimehifadhiwa kwa ajili yao.”