Waziri wa mawasiliano na uchumi dijitali William Kabogo amesema kasi ya mabadiliko katika sekta ya ICT barani Afrika kutokana na maazimio ya kongamano la Connected Africa mwaka jana sio kama vile alitarajia.
Kulingana naye, hatua hii inatokana na ukweli kwamba hakukuwa na jukwaa la ufuatiliaji, ili kufahamu hatua ambazo zimepigwa katika kila nchi na changamoto zilizopo.
Akizungumza na mwanahabari wa KBC, O’Brien Kimani pembezoni mwa kongamano la mwaka huu la Connected Africa huko Diani kaunti ya Kwale, Kabogo amesema kwamba hilo sasa limesahihishwa.
Waziri huyo alielezea kwamba sasa sekretarieti imeundwa na itakuwa jukwaa bora la mawasiliano hata mtandaoni kufuatilia hatua zinazopigwa badala ya kusubiri awamu ijayo ya kongamano hilo.
Kabogo alisema pia kwamba lengo kuu ni kuhakikisha kwamba Bara Afrika limewekwa katika ramani ya ulimwengu kuhusiana na masuala ya teknolojia ya mawasiliano.
Alilalamikia hali ya maeneo mengi barani Afrika ya kukosa miunganisho hitajika kiasi kwamba hayana huduma za msingi za mtandaoni kama ile ya kutuma na kupokea pesa.
“Maeneo ya mashinani Afrika hayajaunganishwa, mengine hata huduma za kutuma na kupokea pesa hakuna, tunasema kampuni kama Safaricom inaweza kufika katika maeneo hayo,” alisema Kabogo.
Changamoto kubwa kulingana na waziri huyo ni miundombinu ya teknolojia akitaja gharama kubwa ya uunganishaji wa nyaya za intaneti ambapo alisema hata Kenya haijaafikia malengo yake.
Waziri huyo aliye mwingi wa matumaini alipongeza wabunge kwa kujitolea kujenga vituo dijitali kwa kutumia pesa za hazina ya maendeleo ya maeneo bunge.
Hatua hiyo anasema inaweka matumaini ya kuwa na kituo cha kidijitali katika kila wadi nchini katika muda wa miaka miwili ijayo.
“Tunataka kuwekwa katika ramani ya ulimwengu kidijitali kwamba watoto wa Kenya wanaweza kuwa katika kiwango sawa na watoto wa Uchina,” alimalizia waziri Kabogo