Waziri Duale na Kibagendi wazozana kuhusu SHA

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa Afya Aden Duale leo amezozana na mbunge wa Kitutu Chache Anthony Kibagendi katika kikao cha kamati ya bunge kuhusu Afya.

Kulingana na video zilizosambaa mitandaoni, Kibagendi alianza kwa kumlaumu waziri Duale kwa kudunisha wanachama wa kamati hiyo kwenye majibu, taarifa zake na hata tabia yake.

Duale kwa upande wake alimfokea Kibagendi akisema kwamba amefunga hospitali zake zilizopatikana zikishiriki ulaghai katika madai ya malipo kutoka kwa halmashauri ya afya ya jamii SHA.

Waziri huyo alisema kwamba Kibagendi hafai kuwa mwanachama wa kamati ya afya kutokana na kile alichokitaja kuwa mkinzano wa maslahi.

Kibagendi alikanusha madai ya Duale kwamba anamiliki hospitali.

Katika taarifa rasmi, wizara ya Afya haikugusia mzozano huo bali iliangazia tu kufika kwa waziri Duale mbele ya kamati hiyo na dhamira ya kufanya hivyo.

Taarifa hiyo ilielezea kwamba Duale alifika kujadili mapendekezo ya kamati hiyo inayoongozwa na mbunge wa Seme James Nyikal, kuhusu ripoti ya utathmini wa halmashauri ya Afya ya jamii SHA.

“Mkutano huo uliangazia pakubwa masuala sita makuu yaliyo kwenye ripoti hiyo, likiwemo suala la kulipa mara moja maombi yaliyowasilishwa ya malipo” ilisema taarifa ya wizara ya Afya.

Duale alielezea kuhusu hatua ambazo SHA imepiga katika kuafiia viwango vya malipo kupitia mchakato wa uhakiki, uhamasisho wa mara kwa mara kwa wanaotoa huduma na uimarishajihi wa mifumo ya kutoa malipo ili kupunguza mrundiko.

Share This Article