Waziri Duale kufuata katiba katika uhamisho wa mishahara ya wafanyakazi wa UHC

Waziri Duale alisema kwamba jukumu la Afya limegatuliwa kulingana na katiba na hivyo atafuata sheria katika kuhamisha mishahara hiyo.

Marion Bosire
1 Min Read

Waziri wa Afya Aden Duale, leo amesisitiza kwa msimamo thabiti kujitolea kwake kutekeleza Katiba kwa kusisitiza umuhimu wa kuhamisha mishahara na bajeti zinazohusiana na wafanyakazi wa huduma ya afya kwa wote – UHC kutoka kwa wizara ya afya hadi kwa serikali za kaunti.

“Afya ni jukumu lililogatuliwa. Sitakiuka Katiba,” alisema waziri huyo, akieleza kwa uwazi heshima yake kwa sheria na dhamira ya ugatuzi.

Duale alitoa kauli hiyo katika jumba la Afya House jijini Nairobi, wakati wa uzinduzi wa vifaa 2,000 vya baridi vilivyotolewa na shirika la watoto la Umoja wa Mataifa -UNICEF.

Vifaa hivyo vitasambazwa kwa kaunti zote 47 ili kuboresha upatikanaji wa huduma za chanjo, ambayo ni sehemu muhimu ya Huduma ya Afya ya Msingi na nguzo kuu ya UHC.

Hafla hiyo pia ilionyesha dhamira ya Serikali katika kuimarisha usambazaji wa chanjo hadi ngazi ya mwisho, kuhakikisha kila mtoto, bila kujali aliko, analindwa dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

Matamshi ya Duale yalijiri wakati ambapo wafanyakazi wa UHC walikuwa wanapanga kuwasilisha malalamiko yao kwa bunge na wizara ya fedha kuhusu masharti ya ajira yao.

Share This Article