Waziri Duale azionya asasi za kudhibiti sekta ya afya

Martin Mwanje
1 Min Read
Waziri Aden Duale akiwa kwenye mkutano na uongozi wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya

Waziri wa Afya Aden Duale ametoa onyo kali kwa asasi za kudhibiti sekta ya afya nchini akizitaka kamwe kutolegeza masharti katika utendaji kazi wake. 

Amesema kuhakikisha usalama wa wagonjwa kunahitaji kuzingatia kikamilifu viwango vya mafunzo vilivyowekwa na Baraza la Wahudumu wa Afya na Madaktari wa Meno nchini (KMPDC).

Waziri ameelezea mashaka kwa kutoa mfano wa kozi ya Shahada ya Sayansi katika Afya ya Mdomo inayotolewa na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) ambayo alisema haikidhi viwango vilivyowekwa na KMPDC.

Si hayo tu, aligusia changamoto zingine zinazoikumba sekta ya afya nchini ikiwa ni pamoja kugeuzwa mafunzo ya tiba kuwa biashara, kuanzishwa kwa kozi ambazo hazijaidhinishwa na mitaala isiyokidhi viwango vinavyohitajika.

Hata hivyo, alisema Wizara yake inafanya kila iwezalo kuzipiga dafrau changamoto hizi wakati ikiimarisha ushirikiano na taasisi za mafunzo kupitia upya mitaala na kuendeleza vitivo miongoni mwa mambo mengine.

Duale aliyasema hayo leo Jumanne wakati wa mkutano na uongozi wa MKU.

 

Share This Article