Waziri wa Afya Aden Duale amekiri kuwa vifo vya kina mama wajawazito vimekuwa vikiongezeka kwa kasi nchini Kenya, na kutaja hali hiyo kuwa ya kusikitisha na isiyokubalika.
Akizungumza mjini Rumuruti, kaunti ya Laikipia, Duale alieleza masikitiko yake kuhusu idadi kubwa ya wanawake wanaofariki kutokana na matatizo ya uzazi.
“Kama Waziri wa Afya, pamoja na Mheshimiwa Rais, hatufurahishwi na hali hii ambapo wanawake wanapoteza maisha wakijifungua. Katika takriban kaunti 27, vifo vingi vya wanawake vinahusiana moja kwa moja na matatizo ya uzazi. Hatuwezi kukubali hali hii iendelee,” alisema Duale.
Alisisitiza kuwa serikali imefanya suala hilo kuwa ajenda ya kitaifa, na itahusisha viongozi wanawake kutoka kila kona ya nchi kutafuta suluhisho.
“Iwe ni hospitali za umma au binafsi, vifo vya uzazi lazima vikome. Hili ni mojawapo ya masuala muhimu ambayo nitashughulikia kama Waziri wa Afya,” aliongeza.
Waziri Duale alitaja kuwa baadhi ya vifo hivyo vinasababishwa na uzembe wa wahudumu wa afya pamoja na miundombinu duni katika vituo vya afya.
“Baadhi ya vifo hivi vinatokana na uzembe wa moja kwa moja au mifumo duni ya afya. Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) inahudumia wajawazito katika hospitali za ngazi ya tatu hadi ya sita — ambapo wengi hujifungulia — lakini kiwango cha sasa cha vifo vya uzazi nchini ni cha kutisha. Ni kinyume cha maadili, ni kinyume cha katiba, na hatuwezi kuendelea kama kawaida,” alisisitiza Duale.
Alihitimisha kwa kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka akisema: “Hatua lazima zichukuliwe — na zichukuliwe sasa!”