Maafisa wa polisi wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI, wamewakamata washukiwa wawili wanaodaiwa kuendesha taasisi ambazo hazijaidhinishwa, na utoaji wa vyeti bandia vya shahada.
Washukiwa hao Moses Masiga, ambaye ndiye Chansela wa Chuo Kikuu cha North Western Christian ambacho kinahusishwa na Power International Ministries University Inc., pamoja naibu Chansela Jackson Khayamba, walikamatwa baada ya Tume ya Elimu ya Juu kulalamika kuhusu kuwepo kwa taasisi ambazo hazijaidhinishwa kutoa vyeti vya shahada.
Hatua hiyo ilisababisha maafisa wa DCI kutekeleza operesheni hadi katika eneo la Wild Waters Nyali.
Walipowasili walilakiwa na sherehe ya mahafali iliyokuwa ikiendelea, huku wanafunzi wakiwa tayari kukabidhiwa vyeti vya shahada.
Maafisa hao walinasa vyeti kadhaa vikiwemo vya shahada, stashahada na uzamifu miongoni mwa vingine, tayari kukabidhiwa mahafali ambao hawakuwa na ufamahu ni vyeti ambavyo havijaidhinishwa na Tume ya Elimu ya Juu.
Washukiwa hao wanazuiliwa na maafisa wa polisi, wakisubiri kufikishwa mahakamani kufunguliwa mashtaka ya kutoa vyeti vya shshada bila idhini, kinyume na sehemu ya 28 ya sheria za Vyuo Vikuu.