Wavuvi na wahudumu wa baharini wakabidhiwa boti na vifaa vya uvuvi Kwale

Martin Mwanje
1 Min Read

Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani amewakabidhi wavuvi na wahudumu wa baharini boti mbili, vifaa vya uvuvi na majokofu ya kuhifadhia samaki ili kupiga jeki sekta ya uvuvi na uchumi samawati katika eneo la Tiwi, gatuzi dogo la Matuga.

Kufikia sasa, serikali ya kaunti hiyo imekabidhi zaidi ya boti 50 za uvuvi na utalii pamoja na vifaa vya ubaharia kwa makundi ya usimamizi wa fuo za bahari na ujenzi wa bandari ndogo 9, ikiwemo ya Tsunza, Waa, Tiwi, Mwaepe, Gazi na Shimoni.

Akihutubu wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Achani amesema serikali ya kaunti itahakikisha kuwa wavuvi wanapata mazingira mazuri ya kuendeshea shughuli zao.

Wakati uo huo, kiongozi huyo ameyahimiza makundi ya usimamizi wa fuo za bahari (BMUs) kuunda kampuni ili waweze kupata zabuni za serikali ya kaunti na mashirika ya kibinafsi.

Kwa upande wao, wakaazi wa Tiwi wakiongozwa na Abdhalla Tendegwa, wameipongeza hatua ya serikali ya Kwale wakiutaja mradi huo kama njia moja ya kubadili hali ya maisha yao.

 

TAGGED:
Share This Article