Chama cha kitaifa cha wauguzi na wakunga hapa nchini (KNUNM), kimeshikilia kuwa mgomo wa kitaifa uliopangwa kuanza Julai 7, 2025 ungalipo.
Katibu Mkuu wa chama hicho Seth Panyako, ameandaa mkutano wa kitaifa wa Baraza la Ushauri Ijumaa ijayo, kuthibitisha ilani iliyotolewa mapema mwezi huu kwa serikali za kaunti na ile ya taifa akitaja maswala ambayo hayajashughulikiwa.
Chama hicho kilielezea wasiwasi kwamba serikali bado haijashughulikia maswala tisa muhimu yaliyoorodheshwa kwenye ilani hiyo ya mgomo ya siku 26.
Kulingana na chama hicho, wauguzi wanaendelea kufanya kazi katika mazingira duni, ambayo yamesababisha kutokuwa na usawa katika uajiri na ukosefu wa usalama kwa mfumo wa Afya ya Umma.
Miongoni mwa maswala yalioibuliwa kwenye ilani hiyo ni kuwaajiri wauguzi kwa ajira ya kudumu.