Serikali ya kaunti ya Kilifi imetoa wito kwa wauguzi wanaoshiriki mgomo kurejea kazini.
Mgomo huo ambao umeingia siku ya tatu leo Ijumaa umedumaza utoaji huduma katika hospitali nyingi za umma katika kaunti hiyo.
Wauguzi hao walisusia kazi kuanzia juzi Jumatano wakilalamikia masuala mbalimbali ikiwemo mazingira mabovu ya kufanyia kazi.
“Tunatoa wito kwa manesi wanaogoma kurejea kazini mara moja na kushiriki mazungumzo yenye tija kupitia njia zilizowekwa ili kusuluhisha malalamiko yao,” alisema Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro kupitia msemaji wake Jonathan Mativo kwenye taarifa.
“Serikali ya kaunti bado iko tayari kwa mazungumzo, lakini hili linapaswa kufanyika ndani ya misingi ya sheria na taratibu zilizowekwa za masuala ya kazi.”
Katika hospitali nyingi za umma, ikiwemo hospitali ya rufaa ya Kilifi, wagonjwa walionekana wakihangaika si haba, na maji yalipozidi unga, walifunga virago na kurejea makwao baada ya kukosa kuhudumiwa.
Kwa upande wao, madaktari walionekana wakishughulikia tu hali za dharura.