Wauguzi waandamana Nyahururu wakitaka ajira ya kudumu

Wauguzi hao walimlaumu Gavana Joshua Irungu kwa kupuuza kilio chao licha ya makubaliano ya kurejea kazini yaliyofikiwa mapema mwezi Januari mwaka huu.

Marion Bosire
2 Min Read

Wauguzi kutoka Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nyahururu waliandamana mjini Nyahururu siku ya Jumatano wakilalamikia kile walichokiita ni kushindwa kwa serikali ya kaunti ya Laikipia kuwapatia ajira ya kudumu na yenye mafao.

Wauguzi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN), Tawi la Laikipia, Bw. Peter Ndiba, walimlaumu Gavana Joshua Irungu kwa kupuuza kilio chao licha ya makubaliano ya kurejea kazini yaliyofikiwa mapema mwezi Januari mwaka huu.

Bw. Ndiba alisema kuwa wauguzi wanamtaka gavana atimize ahadi yake ya kuhakikisha kuwa wauguzi wa mkataba wameajiriwa kwa masharti ya kudumu na yenye mafao, pamoja na ahadi nyingine walizopewa.

Alisisitiza kuwa Gavana Irungu aliahidi kuwaajiri wauguzi wote walioko chini ya kandarasi, lakini hadi sasa baada ya miezi minne, hakuna matumaini yoyote ya utekelezaji wa ahadi hizo.

Mwenyekiti huyo pia alibainisha kuwa kati ya ahadi 11 zilizowekwa kwenye makubaliano ya kurejea kazini mwezi Januari, hakuna hata moja iliyotekelezwa, akiilaumu serikali ya kaunti kwa kupuuza matatizo yanayowakumba wauguzi wa kandarasi.

Katibu wa KNUN, Tawi la Laikipia, Bw. Daniel Wangai alisema kuwa asilimia 80 ya wauguzi katika Kaunti ya Laikipia ni wa mkataba, ambao serikali ya kaunti kupitia makubaliano ya Januari iliahidi kuwa wataajiriwa kwa masharti ya kudumu na yenye mafao.

Bw. Wangai alieleza masikitiko kuwa hadi sasa tangu Januari, serikali ya kaunti haijatimiza ahadi hiyo, ikitaja kiwango kikubwa cha mshahara wa watumishi (wage bill) ambacho kwa sasa kinasemekana kufikia asilimia 55.

Alishangaa ni kwa nini wage bill iwe juu ilhali wauguzi wengi ni wa mkataba na hupokea mishahara midogo.

Mweka hazina wa KNUN, Tawi la Laikipia, Bi. Spelanza Wambui alisema wagonjwa wengi wanateseka hospitalini si kwa makosa yao wala ya wauguzi, bali ni kutokana na kushindwa kwa serikali ya kaunti kutimiza ahadi zake.

KNUN, Tawi la Laikipia wamesema wako tayari kurejea kazini mara tu ahadi zote 11 walizokubaliana mapema mwaka huu zitakapotekelezwa.

Share This Article