Watumishi watatu wa umma washtakiwa kwa kughushi vyeti

Martin Mwanje
3 Min Read

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imewashtaki mahakamani maafisa watatu wa utumishi wa umma kuhusiana ma mashtaka mbalimbali yanayohusiana na kughushi vyeti vya masomo.

Hii ni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kukubaliana na mapendekezo ya tume hiyo kuwashtaki washukiwa hao.

Watatu hao, Kenneth Kiplangat Tonui, Joseph Kihara Kaburugu na Stacey Mwikali Mbati, wanatuhumiwa kutumia vyeti hivyo kupata ajira au kupandishwa vyeo. 

Washukiwa walitumia vyeti hivyo kupata ajira katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na kampuni ya Maji na Taka ya Nairobi City (NCWSC).

 Mshukiwa wa kwanza, Tonui, anatuhumiwa kwa kutumia vyeti ghushi kupata ajira katika IEBC. Alikanusha mashtaka hayo alipofikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Kupambana na Ufisadi ya Milimani Celesa Okore January 24, 2025. Aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi 500,000 na mdhamini wa kiasi kama hicho au shilingi 100,000 pesa taslimu. Kesi dhidi yake itatajwa  Februari 6, 2025. 2.

Mshukiwa wa pili, Kaburugu, ni msimamizi wa michezo katika kampuni ya NCWSC. Anatuhumiwa kwa kughushi cheti cha stashahada ya usimamizi wa sayansi ya michezo katika Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT). Naye pia alifikishwa katika mahakama hiyo Januari 21 na kukanusha mashtaka. Hakimu Mkuu Harrison Barasa alimwachilia kwa dhamana ya shilingi 500,000 na mdhamini wa kiasi kama hicho au shilingi laki moja pesa taslimu. Kesi dhidi yake itatajwa Februari 4, 2025. 

Mshukiwa wa tatu, Mbati, ni afisa wa ICT katika kampuni ya NCWSC. Anatuhumiwa kwa kutumia shahada ghushi ya Teknolojia ya Habari aliyodai ilitolewa na JKUAT. January 23, 2025, alishtakiwa kwa kujipatia mali ya umma kwa udanganyifu, kughushi na kutumia waraka wa uongo na kumdanganya Hakimu Mkuu Harrison Barasa. Mwikali alikanusha mashtaka hayo na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi 500,000 na mdhamini wa kiasi kama hicho au shilingi 100,000 pesa taslimu. Kesi dhidi yake itatajwa Februari 5, 2025.

EACC imeimarisha msako dhidi ya watumishi wa umma waliotumia vyeti ghushi kupata ajira na imetaka wahusika kurejesha fedha zote walizolipwa kwa kipindi walichohudumu punde baada ya wao kupatwa na hatia na mahakama.

Share This Article