Watu wawili wafariki kwenye ajali katika daraja la Nithi

Tom Mathinji
1 Min Read
Watu wawili wafariki kwenye ajali katika daraja la Nithi.

Watu wawili wamefariki kufuatia ajali ya barabarani, iliyotokea katika daraja hatari la Nithi, kaunti ya Tharaka Nithi.

Akithibitisha ajali hiyo, Kamanda wa Polisi kaunti ya Tharaka Nithi Zacheus Ng’eno, alisema ajali ilihusisha Lori hilo lililokuwa likisafirisha ndizi kutoka Meru hadi Nairobi.

Dereva wa Lori hilo anadaiwa kupoteza mwelekeo na kutumbukia mtoni.

“Tayari tumefanikiwa kutoa mwili mmoja, huku mwingine ukiwa bado umebanwa kwenye mabaki ya lori hilo,” alisema Ng’eno.

Mwili huo ulipelekewa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Chuka.

Ng’eno aliwahimiza madereva kuzingatia sheria za trafiki wanapokaribia daraja hilo, ili kuzuia ajali, huku shughuli za ukarabati wa daraja hilo zikitarajiwa kuanza.

Ajali hiyo imetokea siku chache baada ya Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, kuhakikishia wakazi wa eneo hilo kwamba serikali imetenfa shilingi Bilioni nane kwa upanuzi wa daraja hilo.

Daraja hilo ambalo linaunganisha kaunti za Meru na Tharaka Nithi, limeshuhudia ajali kadhaa kwa muda wa miaka mingi hali inayoibua wasiwasi kuhusu usalama wa wasafiri na wakazi kwa jumla.

TAGGED:
Share This Article