Watu wawili ambao wanapokea matibabu katika hospitali ya Kangundo Level 4 kaunti ya Machakos, wamedhibitishwa kuambukizwa virusi vya ugonjwa wa Monkey Pox almaarufu Mpox, na wametengwa kutoka wagonjwa wengine.
Msimamizi wa hospitali hiyo Juliet Munyao, alisema wawili hao waligunduliwa na dalili za ugonjwa huo siku ya Ijumaa iliyopita. Sampuli zao zilipelekwa kwenye maabara ambapo uchunguzi ulibaini kuwa wameambukizwa virusi hivyo.
Juliet aliwahakikishia wakazi kuwa hatua madhubuti zimechukuliwa na kwamba wagonjwa hao wataendelea kupokea matibabu.
Afisa wa afya ya umma huko Kangundo Fredrick Kimemia,pia amewataka wakaazi wa sehemu hiyo kuzingatia maagizo ya kiafya ili kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.