Watu watatu wafariki baada ya kituo cha polisi kuteketezwa Nyandarua

Tom Mathinji
1 Min Read
Kituo cha polisi cha Ndunyu Njeru kaunti ya Nyandarua chateketezwa.

Washukiwa watatu wa wizi wa mifugo, wameaga dunia baada ya wakazi waliojawa na hasira kuteketeza kituo cha polisi cha Ndunyu Njeru katika kaunti ya Nyandarua Alhamisi usiku.

Kulingana na naibu kamishna wa  kaunti ndogo ya Nyandarua ya kati Michael Ololtuaa,washukiwa hao walikuwa wakizuiliwa katika korokoro ya kituo hicho cha polisi  wakati wakazi walipokiteketeza mwendo wa saa mbili usiku.

Kisa hicho kilifuatia taharuki ya mchana kutwa katika sehemu hiyo, iliyosababishwa na kisa ambapo polisi alimuua kwa kumpiga risasi mwandamanaji mmoja wakati wa maandamano hayo ya kulalamikia ongezeko la visa vya wizi wa mifugo.

Ghasia zilianza baada ya wakazi hao kuwakamata washukiwa hao watatu na kuwakabidhi kwa polisi. Lakini hasira yao iliongezeka kufuatia madai kwamba washukiwa hao walikuwa wakishirikiana na polisi kuhusiana na wizi huo wa mifugo.

Miili ya washukiwa hao watatu inahifadhiwa katika makafani ya hospitali ya  Engineer.

TAGGED:
Share This Article