Watu wanne wamefariki na mwingine kujeruhiwa baada ya jamii mbili kuzozana katika eneo bunge la North Horr, kaunti ya Marsabit.
Wanne hao ambao wote ni wanaume,wametoka katika jamii za wafugaji za Gabra na Wayu, waliuawa kwa kupigwa risasi wakati wa ghasia hizo.
Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), imeanzisha uchunguzi kubainisha chanzo cha mzozo huo.
Akithibitisha kisa hicho, Kamishna wa kaunti ya Marsabit James Kamau, huku akiwaonya wakazi dhidi ya kuchukua hatua mikononi mwao, alisema uhasama huo ulichochewa baada ya kupatikana kwa miili miwili ya vijana wa jamii ya Gabra katika eneo la Qorta, ambao walikuwa wametoweka.
Kulingana na Kamau aliyezungumza na wanahabari baada ya kuongoza mkutano wa kiusalama, alisema jamii ya Gabra ilitekeleza shambulizi la kulipiza kisasi katika eneo la Manyatta na kuwaua watu wawili wa jamii ya Wayu.
Mwanamke mmoja alipata majeraha ya risasi wakati wa shambulizi hilo, na yuko katika hali nzuri .
Aidha Kamishna huyo wa kaunti alisema mwanasiasa mmoja wa eneo hilo anafuatiliwa kwa karibu na maafisa wa DCI, kwa madai alichochea na kufadhili uvamizi huo.
“Maafisa wa usalama wamepewa maagizo kuhusu orodha ya washukiwa 26, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha washukiwa hao wanahojiwa na polisi,’ alisema Kamau.
Alikuwa ameandamana na Kamanda wa polisi wa kaunti hiyo Lenard Kimaiyo miongoni mwa viongozi wengine wa eneo hilo.