Watu wasiopungua saba wameuawa na wengine 20 kujeruhiwa katika shambulio dhidi ya hospitali mmoja nchini Sudan Kusini, haya ni kulingana na shirika lisilo la kiserikali la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF).
Haya yanajiri wakati ambapo hofu inaongezeka kwamba taifa hilo changa zaidi duniani linaweza kurejea tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Shirika la MSF limelaani vikali kushambuliwa kwa hospitali yake kwa makusudi katika eneo la Old Fangak siku ya Jumamosi na kuelezea kwamba shambulio hilo lilibomoa hospitali na duka la dawa la mwisho lililokuwa likihudumu kaskazini mwa nchi hiyo.
MSF ilitoa wito kupitia ukurasa wake wa X wa kuhimiza wahusika waachane na mabomu, walinde raia pamoja na huduma za Afya ikitaja shambulio hilo kuwa ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Haijafahamika mara moja ni kwa nini kituo hicho cha afya kililengwa. Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini hakupatikana ili atoe maoni, kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press.
Mamman Mustapha mkuu wa ujumbe wa MSF nchini Sudan Kusini, aliambia Al Jazeera kutoka mji mkuu Juba kuwa wanachama wake walio katika eneo la tukio waliripoti kwamba helikopta mbili za kijeshi zilishambulia hospitali hiyo.
Mustapha alisema helikopta hizo zilirusha mabomu katika hospitali na vifaa vyake vya matibabu na kisha kuendelea kulishambulia eneo la Old Fangak.
“Wakazi wote wamekimbia na hali ni mbaya sana na ya kutisha. Tumeshangazwa sana. Hospitali hiyo imekuwepo kwa miaka 10, tangu mwaka 2014” alisema Mustapha.
Taarifa nyingine ya MSF ilielezea kwamba shambulio lilianza saa kumi unusu alfajiri na mabomu hayo yalisababisha moto ulioteketeza hospitali hiyo.
Mashambulizi mengine yalifanyika saa kadhaa baadaye karibu na soko katika mji huo wa Old Fangak, na kusababisha hofu kubwa na wakazi kukimbia makazi yao, kwa mujibu wa mashuhuda kadhaa.
Umoja wa Mataifa umetahadharisha katika wiki za hivi karibuni kuwa Sudan Kusini, ambayo imekumbwa na hali ya kutokuwa na utulivu tangu ilipopata uhuru kutoka Sudan mwaka 2011, iko hatarini kurejea tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Nchi hiyo imetumbukia kwenye mzozo katika miezi ya hivi karibuni kufuatia kuvunjika kwa makubaliano ya kugawana madaraka kati ya majenerali hasimu, Rais Salva Kiir na Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar.
Kiir na Machar wanatoka katika makabila mawili makubwa zaidi, yaani Dinka na Nuer mtawalia, ambayo yalipigana vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya 2013 na 2018 vilivyosababisha vifo vya watu takriban 400,000 kabla ya makubaliano ya amani ya mwaka 2018 kuwawezesha viongozi hao kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Hivi sasa, mvutano kati ya Kiir na Machar umefikia kilele, huku Machar akiwa amewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani tangu Machi kwa tuhuma za njama ya kuhujumu serikali.
Old Fangak, ambako hospitali ya MSF ilishambuliwa, ni mojawapo ya miji mikubwa katika wilaya ya Fangak, Jimbo la Jonglei, eneo linalokaliwa na watu wa kabila la Nuer na ambalo kihistoria linahusishwa na chama cha Machar, Sudan People’s Liberation Movement-in-Opposition (SPLM-IO).