Watu wengine tisa wamethibitishwa kuambukizwa ugonjwa wa Mpox hapa nchini, huku idadi jumla ya maambukizi ya ugonjwa huo ikifika 137.
Kulingana na wizara ya Afya, visa vipya vya maambukizi ya ugonjwa huo vimeripotiwa katika eneo la usafiri la Kaskazini ambazo ni Busia (48), Mombasa (37), Nakuru (16), Makueni (10), Nairobi (5), Kajiado (3), Bungoma (3), Taita Taveta (2), Kericho (2), Kilifi (2), Kiambu (1), Uasin Gishu (1), Migori (1), Machakos (2), Isiolo (1), Kisii (1) na Kirinyaga (1).
Katibu wa idara ya Afya ya Umma Mary Muthoni, alidokeza kuwa jumla ya watu 400 waliotangamana na waathiriwa wametambuliwa huku 315 kati yao wakichunguzwa kwa kipindi kinachohitajika cha siku 21. Kati ya hao, watu tisa walibainshwa kuambukizwa ugonjwa wa Mpox.
“Zaidi ya watu Milioni 4.8 wamechunguzwa katika sehemu za mpakani, na wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa hufanyiwa uchunguzi zaidi. Hadi sasa sampuli 597 zimechunguzwa na 137 zimebainishwa kuwa na Mpox,” alisema Muthoni kupitia kwa taarifa.
Kwa mujibu wa Muthoni, Ili kuimarisha juhudi za kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo, wizara ya Afya kwa ushirikiano na serikali za kaunti na washirika wengine wameboresha mifumo ya uchunguzi, kuwaorodhesha waliotangamana na waathiriwa na utoaji mafunzo.