Watu 13 wauawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza

Martin Mwanje
1 Min Read
Israel imeanzisha mashambulizi mapya katika Ukanda wa Gaza

Mamlaka ya Ulinzi wa Raia katika eneo la Gaza leo Jumatano imesema kuwa watu 13 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel katika eneo hilo la Palestina tangu usiku wa manane.

Israel “ilifanya mashambulizi kadhaa ya anga… yaliyosababisha vifo vya watu 13 na kujeruhi makumi, wakiwemo wanawake na watoto, mjini Khan Yunes na Jijini Gaza”, Mahmud Bassal, msemaji wa mamlaka hiyo aliiambia AFP.

Jana Jumanne, Israel ilianzisha mashambulizi yake makubwa zaidi katika Ukanda wa Gaza tangu kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha vita Januari 19 kati yake na wanamgambo wa Kipalestina wa Hamas ili kumaliza vita vya zaidi ya miezi 15.

Mashambulizi hayo, yaliyokuja baada ya kusambaratika kwa mazungumzo ya kurefusha makubaliano hayo, yaliua watu zaidi ya 400, ilisema Wizara ya Afya katika eneo hilo linaloendeshwa na Hamas.

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alionya jana Jumanne kuwa mashambulizi hayo “yalikuwa mwanzo tu” na kwamba mazungumzo ya siku zijazo na Hamas “yatafanyika tu chini ya mashambulizi makali”.

“Hamas tayari imehisi nguvu ya mkono wetu katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Na ninataka kukuahidi  –- na wao –- huu ni mwanzo tu,” aliongeza Netanyahu katika taarifa ya video.

 

TAGGED:
Share This Article