Watu 11 wameripotiwa kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa jana Alhamisi wakati mlipuko ulipotokea katika mji wa Bukavu unaopatikana mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).
Mlipuko huo ulitokea wakati wa mkutano wa hadhara ulioongozwa na viongozi wa kundi la M23 na kuwaacha watu wengi wakiwa wamejeruhiwa na kuvuja damu.
Kundi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda lilichukua udhibiti wa mji huo mapema mwezi huu.
Viongozi wa kundi hilo wameishutumu serikali ya DRC kwa kutekeleza shambulizi hilo la bomu. Wanadai washambuliaji ni miongoni mwa waliouawa kwenye mlipuko huo.
Rais wa DRC Felix Tshisekedi amewatuhumu “wanajeshi wa kigeni” ambao hakuwataja kwa majina kwa kutekeleza shambulizi hilo.
“Shambulizi hilo lilisababisha vifo vya watu 11 na uchunguzi unaendelea.,” Corneille Nangaa, kiongozi wa muungano wa Congo River Alliance (AFC) aliwaambia wanahabari. Muungano huo unajumuisha M23.
“Watu 65 walijeruhiwa, baadhi yao vibaya zaidi, na wanapokea matibabu katika chumba cha upasuaji.”