Huduma ya Taifa ya Polisi (NPS), imesema watu 11 wamefariki huku maafisa 52 na raia 11 wakijeruhiwa kwenye maandamano ya Saba Saba yaliyofanyika Jumatatu hapa nchini.
Kupitia kwa taarifa, Msemaji wa Huduma ya Taifa ya Polisi Muchiri Nyaga, alisema zaidi ya watu 567 wametiwa mbaroni akiwemo mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji kwa kujihusisha na shughuli za uhalifu.
Kwenye taarifa hiyo ya awali kuhusu maandamano hayo, NPS pia iliripoti visa vya uharibifu wa mali unaojumuish magari 12 ya polisi, magari matatu ya serikali na manne ya wananchi.
“Baadhi ya watu walijihusisha na visa vya uhalifu na uvunjaji wa sheria, vilivyojumuisha kuwashambulia maafisa wa usalama na uporaji wa mali,”alisema Msemaji huyo wa Polisi.
Hata hivyo, NPS iliwapongeza wengi wa wakenya ambao walidumisha amani, kuzingatia sheria na utulivu.
Huduma hiyo ya Polisi ilisema kuwa inachunguza visa hivyo vyote na kuhakikishia umma waliohusika na visa vya uhalifu watachukuliwa hatua.
“Huduma ya Taifa ya Polisi inatoa wito kwa yeyote aliye na habari kuhusu watu waliojihusisha na visa vya uhalifu kuripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu,”ilisema taarifa hiyo.