Watu kumi walifariki jana Jumamosi kwenye ajali mbaya ya barabarani katika eneo la Mai Mahiu huku wengine wakiachwa na majeraha.
Ajali hiyo ya saa sita mchana ilihusisha trela na gari la kubeba abiria 14.
Walioshuhudia walisema kwamba trela ilipoteza mwelekeo kabla ya kugonga gari hilo la abiria ambayo lilikuwa limejaa abiria. OCPD wa Naivasha Stephen Kirui alithibitisha ajali hiyo akisema kwamba watu wengine walikimbizwa hospitalini wakiwa na majeraha.
Inaripotiwa kwamba waliokuwa kwenye gari hilo la kubeba abiria ni watu wa familia moja waliokuwa wakienda kuhudhuria hafla ya kifamilia ajali ilipotokea.
Tukio hilo lilisababisha msongamano mkubwa wa magari.